DOKTA MATUZYA ABEBESHWA MSALABA WA TASMA, AFUNGIWA NA KUFUTWA KUJIHUSISHA NA SOKA KISA CHAMA KUTOKUWA NA AKAUNTI YA BENKI

Ofisi ya msajili wa vyama na vilabu vya michezo nchini chini ya Baraza la michezo nchini (BMT) limethibitisha kumfuta na kumfungia kujihusisha na masuala yote ya michezo kwa kipindi kilichobakia Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo Tanzania (TASMA), Dokta Nasoro Matuzya kutokana na chama hicho kukiuka Sheria ya BMT ambayo inavitaka vyama vya michezo kuweka mahesabu na kumbukumbu ya fedha wanazozipata zikiwa katika usahihi unaokodhi viwango vya mahesabu.



Kaimu Msajili wa Vyama vya michezo nchini Ibrahim Mkwawa amesema, Mara baada ya Ofisi ya msajili kutuma wakaguzi wa kugundua mapungufu yaliyopo ndani ya ofisi hiyo walichukua hatua zinazostahiki
"Ofisi ya msajili ilituma wakaguzi na walikwenda kukagua kwenye ofisi za TASMA ambapo walijiridhisha kwamba TASMA inaendesha shughuli zake bila kuwa na akaunti ya benki, akaunti iliyokuwepo ilisitishwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa, " amesema.



"Kwahiyo baada ya kubaini hilo kwa mujibu wa Baraza la michezo la Taifa, msajili kwa mamlaka aliyopewa ameamua kuchukua hatua hiyo ya kumfutia uongozi kwa kipindi kilichobakia kwani tunafahamu TASMA hivi karibuni wanafanya uchaguzi wao lakini vilevile tumeamua kumsimamisha kujihusisha na shughuli na shughuli za michezo au uongozi wa mchezo wowote hapa nchini kwa kipindi cha miaka mitatu, " amesema.

Mkwawa ameongeza kwa kuvitaka vyama vingine vya michezo kutokufanya kazi kwa mazoea huku akivitaka vyama vyote vya michezo kuwa mpaka ifikapo Februari 28 mwaka huu viwe vimewasilisha mahesabu yaliyokaguliwa kama sheria inavyotaka kabla hawajachukua sheria.



"Tunavyama takribani 48 vya michezo, tulishavagiza kuleta mahesabu yaliyokaguliwa na mkaguzi anayetambulika, baadhi ya vyama vimetekeleza na baadhi havijatekeleza, na maagizo haya tulitoa tangu Agasti mwaka jana na mpaka sasa ni vyama nane pekee vimetekeleza kwa kuwasilisha mahesabu yao halafu vyama saba vimeandika barua kuomba muda ili waweke mambo yao vizuri kwahiyo hivyo vilivyobakia itakapofika mwisho wa mwezi huu kwa wale ambao hawajatoa taarifa sheria itafata mkondo wake, " amesema.


No comments