Makala:Busungu karibu sebuleni tutazame show ya Olunga


Na:ABDULAH MKEYENGE

NIMESOMA kwenye moja ya mtandao wa kijamii na kuiona stori ya Malimi Busungu akilaani kutofunga bao lolote lile katika michezo ya Ligi Kuu Bara inayokwenda ukingoni.

Busungu amelalamika na kujishangaa juu. Amesema anasaidia sana washambuliaji wengine kupata nafasi za kufunga, lakini yeye ndiyo hafungi.

Nimeshangaa kidogo na kujiuliza ni kweli Busungu ninayemjua ndiyo amejishangaa kutofunga au Busungu mwingine.

Kufunga ni kipaji. Busungu ana kipaji hiki. Amewahi kufunga akiwa Mgambo JKT akafunga tena akiwa na Yanga, inakuwaje leo hii ndani ya Lipuli Fc mabao yamkimbie mpaka ameamua kulalama hadharani?

Busungu amejimaliza na mambo mengi nje ya uwanja. Katika nafasi ambayo inahitaji utimamu wa mwili kwa asilimia 100 ni ushambuliaji.

Nafasi ya ushambuliaji unakutakana na walinzi ambao ndio wanafanya mazoezi magumu kuliko washambuliaji, viungo, mawinga na makipa, utimamu wa mwili mdogo alionao Busungu, lazima aone mabao yamemkimbia.

Nafasi yake wanaume wanaminyana kisawasawa, unadhani unapataje urahisi wa kufunga kama utimamu wako wa mwili mdogo mwilini? Katika hili mchawi wa Busungu ni Busungu mwenyewe. Full stop.

Alivyokuwa Mgambo JKT na baadae Yanga, kuna kitu alikuwa anakitafuta ndiyo maana hakuwa anakauka viwanja vya mazoezi, lakini leo amekuwa mwanadamu wa tofauti kabisa.

Hataki tena kufanya mazoezi magumu, hataki tena kuwahi viwanja vya mazoezi. Mkaidi, mkosefu wa nidhamu. Mchezaji wa namna hii, mabao yanabaki vipi mguuni mwake?

Busungu amejimaliza mwenyewe. Angeongeza bidii pale alipokuja Yanga, leo hii tungekuwa tunazungumza mengine, lakini amebweteka Yanga wakamuacha na sasa yuko zake Lipuli Fc anakolalamika kukimbiwa na mabao.

Wakati Busungu akijishangaa kukimbiwa na mabao, rafikiye Michael Olunga anazidi kusonga mbele. Mwaka 2015 Olunga alikuja nchini na timu yake ya Gor Mahia ya kwao Kenya na kuwasha moto mkubwa katika michuano ya Kagame.

Busungu alikuwa staa wa Yanga, Olunga alikuwa staa wa Gor Mahia. Baada ya michuano ile kumalizika, stori za wachezaji hawa zimebadilika ghafla.

Olunga amekwenda juu, Busungu ameshuka chini. Hivi unavyosoma andiko hili fahamu Olunga ni kati ya Wakenya wanaokipiga La Liga na ndani ya msimu huu amefunga mabao matatu (Hatrick).

Olunga hajafika hapo alipofika kwa makusudi, Busungu hayuko Lipuli Fc kwa bahati mbaya. Kila mmoja amefika alipo kwa juhudi zake mwenyewe.

Muda huu ambao Busungu amejikita kulalama mabao kumkimbia, naomba nimkaribishe sebuleni kwangu tumtazame Olunga ndani ya La Liga. Hakuna namna.

No comments