ASANTE KWASI ‘ANAPOMTUPA’ ZIMBWE JR KATIKA ‘MAJI MAREFU’

Na Baraka Mbolembole
MCHEZO wake wa kwanza tu katika ligi akiichezea Simba alifunga bao.
Na kuanzia hapo amekuwa tishio si tu kwa wachezaji wa timu pinzani bali
hadi kwa mchezaji bora zaidi wa klabu yake msimu uliopita, Mohamed
Hussein ‘Zimbwe Jr.’
Namzungumzia mlinzi ‘kiraka’ raia wa Ghana, Asante Kwasi ambaye
alifunga goli la pili la Simba katika ushindi ‘usiotarajiwa’ 4-0 vs
Singida United mwezi uliopita. Kwasi alifunga goli hilo baada ya kuvunja
mtego wa kuotea uliowekwa na walinzi wa Singida United na kuwahi pasi
ndefu ya mbali iliyopenyezwa na kiungo Said Ndemla.
Ni beki ‘haswa’
Kutokana na mfumo wa kiuchezaji wa Simba-kukaa sana na mpira
nakuanzisha mashambulizi kutokea nyuma kwenda mbele, Kwasi ameweza
kuingia rahisi katika mchezo wa timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa
wa kumiliki mpira, kukaba, kuanzisha mashambulizi na kushambulia kwa
mipira yake mirefu inayofika kwa walengwa.
Kusema kweli, licha ya kwamba tangu kuanza kwa msimu huu, Erasto
Nyoni ameonekana bora katika beki za pembeni lakini katika michezo minne
iliyopita ambayo Simba imecheza ikiwa na Kwasi katika upande wa kushoto
mlinzi huyo ameongeza kitu.
Licha ya kuwa ni ‘chachu’ kwa mashambulizi ya Simba akitokea upande
wa kushoto, uwezo wake wa kucheza katika nafasi na kuziba mianya ya
kupitishwa mpira katika ‘njia’ kwa wachezaji wa timu pinzani
kunanikumbusha baadhi ya walinzi bora zaidi wa kushoto waliopata kutokea
katika timu hiyo katika miaka ya karne mpya.
Kwasi anapora vizuri mpira ikitokea hivyo ila kutokana na mwili wake
wa kawaida yeye amekuwa akitegemea zaidi kuziba njia za wapinzani. Ni
mbabe katika kukaba na uwezo wake wa kucheza nafasi zote za beki ya kati
kumemfanya kuwakumbusha mara kwa mara walinzi wenzake jambo ambalo
limekuwa likiongeza umakini katika timu yao.
Kama mshambuliaji
Baada ya michezo yake minne ya VPL akiwa Simba huku akiwa tayari
amefunga goli moja na kutengeneza mawili likiwemo lile alilofunga
Emmanuel Okwi vs Azam FC siku ya Jumatano hii, bila shaka Mghana huyu
anaacha maswali kuhusu hatma ya Zimbwe Jr ambaye amecheza michezo miwili
tu kati ya 17 ambayo timu yake imecheza msimu huu.
Zimbwe anapaswa kujituma zaidi katika viwanja vya mazoezi ili
kurejesha nafasi ambayo aliiopoteza hata kabla ya ujio wa Kwasi. Alikuwa
‘nguzo’ ya Simba katika beki ya kushoto wakati timu hiyo iliposhinda
Taji la FA msimu uliopita huku yeye akitwaa tuzo ya mchezaj bora wa
klabu na ligi kuu.
Majeraha ambayo aliyapata kwenye mchezo wa fainali ya FA msimu
uliopita yamechangia kumrudisha nyuma nahodha huyo msaidizi wa Simba na
ujio wa Kwasi ni ishara nyingine mbaya kwake kama hatakaza ‘buti’ lake
na kupigania nafasi.
Kwasi anajituma jambo ambalo lipo pia kwa Zimbwe Jr, ila yeye amekuwa
akiangushwa na uwezo wake uleule wa kila siku huku akicheza nafasi moja
tu kwa usahihi. Zimbwe Jr alitengeneza magoli mengi ya Simba msimu
uliopita lakini stahili yake ya kushambulia bila kuzingatia nafasi yake
ya ulinzi inaweza kuendelea kumuangusha kama hatabadilika.
Kwasi tangu yupo Mbao FC msimu uliopita na baadae Lipuli ameonekana
kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa timu pinzani lakini pia amekuwa na
faida ya kufunga magoli kwa timu yake kutokana na uwezo wake wa
kufuatilia mashambulizi yanayotokea nyuma na kuhakikisha anafika katika
eneo ambalo anadhani mpira wa mwisho utafika.
Hii inatokana si tu tamaa ya mchezaji husika katika kushambulia bali
uwezo pia wa kuusoma mchezo na kufanya maamuzi sahihi katika wakati
sahihi. Kushambulia kwake hakumuondolei sifa yake uwanjani mchezaji wa
nafasi ya ulinzi na hii inatokana na umakini ambao amekuwa nao anapokuwa
ndani ya nusu uwanja ya eneo la timu yake.
Zimbwe Jr amtazame Kwasi
Zimbwe Jr ni kati ya wachezaji ambao wanapaswa kuongeza umakini kwa
kiasi kikubwa hasa katika uzuiaji na upigaji wake pasi ili kumuondoa
Kwasi katika nafasi ya beki wa kushoto.
Kuendelea kumuona mchezaji bora wa klabu na VPL msimu uliopita
akishika shavu lake katika benchi ni jambo lisilopendeza lakini katika
mchezo wa soka ni rahisi kupanda kuliko kubaki katika kilele na Zimbwe
Jr asipostuka mapema anaweza kufuata nyayo za wachezaji bora wa msimu
ambao ‘walipotea’ mara tu baada ya kushinda tuzo hiyo. Kwa sasa lazima
tukubali ukweli kuwa Kwasi amemuweka katika ‘maji marefu mno’ Zimbwe Jr
ni wakati wake wa kujiokoa sasa.
Post a Comment