KOCHA WA ZAMANI WA SIMBA AANZA KWA USHINDI HUU NYUMBANI.
WAKATI JKU ya Zanzibar ikianza kwa suluhu dhidi ya Zesco United ya Zambia, Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr ameanza kwa kishindo michuano ya CAF baada ya jana Jumamosi kuifumua Leones Vegetarianos ya Guinea Bissau.
Kerr anayeinoa Gor Mahia alishuhudia vijana wake wakipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kenyatta na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018.
Mabao mawili yakiweka kila moja katika kipindi kimoja, yalitosha kuisaidia K’Ogalo kujiweka pazuri ikihitaji sare tui katika mechi ya marudiani siku 10 zijazo.
Kelvin Omond alianza kuiandikia Gor bao la kuongoza dakika 20 kabla ya mtokea benchi Ephrem Guikan kuongeza la pili dakika ya 60 na kumfanya Kerr aliyetemwa Simba mapema mwaka juzi, kuanza michuano hiyo ya CAF kwa kishindo.
Katika michezo mingine ya Ligi ya Mabingwa JKU ikiwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar ililazimishwa suluhu na Zesco, huku Zanaco FC ya Zambia ikishinda mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Armed Force ya Gambia, Rayon Sport ya Rwanda ililazimishwa sare ya 1-1 na majirani zao wa LLB Academic ya Burundi na KCCA ilikufa ugenini huko Madagascar kwa kulala mabao 2-1 na CNaPS Sports, bao la ushindi likifungwa jioni.

Post a Comment