HATUA YA TISA BORA YA LIGI DARAJA LA TATU JIJINI MWANZA KUANZA MWISHONI MWA MWEZI HUU.
Hatua ya tisa
bora katika ligi daraja la tatu mkoani Mwanza inatarajiwa kuanza
kutimua vumbi kuanzia Februari 26 mwaka huu kwenye uwanja wa kisasa wa
Nyamagana Jijini Mwanza.
Katibu wa
chama cha mpira wa miguu mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake.
Alisema
kamati ya mashindano inatangaza rasmi timu zilizofuzu hatua ya tisa bora
(fainali) kutoka vituo viwili vya Nyehunge na Ngudu huku Nyamagana
wakisubiria kukamilisha michezo ya hatua ya kwanza inayotegemewa
kumalizika Februari 18 mwaka huu.
Malongo
alizitaja timu zilizofuzu kwenye hatua hiyo katika kituo cha Nyehunge
kuwa ni Singa FC yenye pointi 12, Mwanza Ndovu pointi 7, Iseni FC pointi
sita huku kituo cha Ngudu kikiwa na timu ya Igoma Heroes yenye pointi
15, Black Mamba pointi 13 na Vijana FC pointi 11.
Alisema
kamati inaagiza viongozi wa timu ziliofuzu hatua ya fainali ambao ni
Makatibu na timu meneja kuhudhuria kikao cha maandalizi Februari 19
mwaka huu katika uwanja wa CCM Kirumba majira ya saa 04:00 asubuhi kwa
ajili ya kujadiliana, kukumbushana kanuni pamoja na kutoa utaratibu wa
kuboresha ikosi vyao kwani chama kimetoa siku saba za kuongeza na
kusajili wachezaji watano ili kuweza kujiandaa na fainali hiyo.
Hata hivyo alisema wamezishusha daraja timu za Kisesa Star, Igogo FC,
Mwanza City na TSC Academy kutokana na kushindwa kufika
viwanjani pamoja na kujiondoa kwenye mashindano wakati ligi imekwisha
anza.
Sambamba na
hayo alisema wamemfungia mchezaji John Evarist kujihusisha na mpira wa
miguu kwa miezi kumi na mbili baada ya kudanganya jina ili acheze
vilabu viwili kwa wakati mmoja ambavyo ni Singa FC ambapo alitumia jina
la John Evarist huku timu ya Buselesele FC akitumia John Otaka hivyo
kwa mujibu wa kanuni namba 50 (1) imemkataza mchezaji yoyote atakaye
badili jina lake halisi kwa madhumuni ya kudanganya ili asajiliwe na
kwamba akigundulika atafungiwa kucheza mpira ndani na nje ya nchi kwa
kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili kuanzia siku atakayo bainika.
Aidha alisema
timu ya Singa FC imepigwa faini ya Tsh. 800,000 baada ya kumchezesha
mchezaji John Evarist michezo minne na fedha hizo zinatakiwa kulipwa
kabla ya kushiriki hatua inayofuata ya tisa bora ikiwa hiyo ni kwa
mujibu wa kanuni namba 50 (2) inayosema “Klabu iliyo
mchezesha mchezaji aliyebadilisha jina kwa nia ya kudanganya italipa
faini ya Tsh. 200,000 kwa kila mchezo ambao mchezaji huyo alicheza
lakini matokeo hayata badilika”.
Pia aliongeza
kuwa kamati imemfungia Katibu wa Singa FC Eladius Atanas kujihusisha na
masuala ya mpira wa miguu kwa muda wa miezi sita kuanzia Februari 13
mwaka huu kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu mchezaji John Evarist kwa
mujibu wa kanuni namba 50(8) inayosema “ Kiongozi yeyote wa chama cha
mpira wa miguu au kilabu atakayetoa taarifa za uongo na kupotosha chama
cha mpira wa miguu cha mkoa husika katika maamuzi yake kuhusiana na
usajili atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa kipindi kisichopungua
miezi sita.

Post a Comment