SINGIDA UNITED INAKWENDA MBELE NA KURUDI NYUMA.


ILIKUJA kama timu tishio iliyozitisha timu nyingi. Timu inayofundishwa na Hans Van Pluijm, yenye wachezaji wa kariba ya Shaffiq Batambuze, Danny Usengimana, ilimtisha kila mmoja. 


Singida United ilitisha kimtazamo, ilitisha kwa mikataba minono iliyosaini na kufanya jezi zao zichafuke kwa matangazo mbalimbali bado ikaja kututisha ndani ya uwanja kwa kupiga soka la Kiholanzi 'Total football '.

Mashabiki Simba, Yanga walianza kuitazama Singida United kama mshindani wao mwingine kando ya Azam Fc ambaye amekaa katikati yao. Waliihofia sana timu hii. 

Wakati yote yanafanyika, huwezi kuamini ukiambiwa timu hii ndiyo kwanza ilikuwa imepanda daraja la ligi kuu kama ilivyokuwa kwa Njombe Mji na rafiki zangu wa Lipuli Fc. 

Muonekano wa Singida United uliwafanya wasionekane kama timu iliyopanda daraja ambayo mafanikio yake makubwa yanakuwa kubakisha timu isishuke ndani ya msimu mmoja. 

Maisha yao yakawa mazuri. Wachezaji wao wakaishi pepo ndogo ndani ya Singida yenye vijiji vizuri na tulivu kama Itotolo.

Hali yao ikawafanya wasiwekwe katika daraja la Lipuli Fc wala Njombe Mji, haraka kabisa nao wakawa timu inayotajwa kushinda taji. Maisha yameenda kasi sana upande wao. 

Wakaja Ligi Kuu Bara na kila aina ya mbwembwe iliyokolezwa na hamasa ya Singida kwanza. Kashida zote hizi wakaenda katika mchezo wao wa kwanza wa ligi na wakapoteza dhidi ya Mwadui FC pale Mwadui Complex. 

Matokeo hayo yaliwashangaza watu. Kila mmoja alishangaa, inawezekana hata Singida United wenyewe waliyashangaa. Aliyesema mpira una matokeo ya kikatili, hakuwa mbali na ukweli. 

Ni kweli mpira una matokeo ya kikatili.  Yote haya yalionekana si kawaida kutokana na uwekezaji uliofanywa ndani ya Singida United. Unapokuwa na Pluijm kisha ukawa na Batambuze, wewe unakuwa hujaja ligi kuu kutalii kama zinavyotalii timu nyingi ambazo zinaingilia mlango wa mbele kisha zinatokea mlango wa nyuma. 

Wakati ligi ikiwa inakwenda ukingoni, pole pole kabisa kwa mwendo wa madaha Singida United wameamua kujitenga na vigogo. Ni kama maji yanavyojitenga na mafuta katika pipa kubwa. 

Timu yao inaanza kupungua makali. Haitishi tena. Inawezekana wachezaji wamejisahau baada ya kutumia magari mazuri na kulipwa mishahara minono. Inawezekana hili! 

Mwishoni mwa wiki wametoka kufungwa na Stand United tena katika dimba lao la Namfua. Si dhambi wao kufungiwa nyumbani, lakini walikuja na mlengo huu wa kupoteza mechi na timu dhaifu kama Stand United?

Huenda mipango yao mizuri tukaiona msimu ujao, lakini uwekezaji waliofanya msimu huu wanapaswa kumaliza ligi hata nafasi ya pili. Lakini bado siioni nafasi hii jinsi watakavyoipata. 

Inaonekana ni mafanikio makubwa ya wao kusalia kwenye ligi msimu huu ili ujao tuwaone tena, lakini tuambiane ukweli kuwa Singida United hawakuwa na timu ya kubaki katika ligi kisha wakapiga nderemo na vifijo, walikuwa na timu ya kubeba taji, si vinginenyo. 

Muda huu ambao Yanga, Azam Fc zinajikongoja na mpinzani aliyekamilika akionekana kuwa Simba pekee, Singida United wanashindwaje kufanya vyema mfululizo zaidi wana kazi ya kwenda mbele na kurudi nyuma?

No comments