KMC YAIPANIA AZAM FC KESHO ASFC, YASEMA HAWAHOFII WACHEZAJI WAO WAKIMATAIFA

Hatua ya 16 bora mzunguko wa Nne wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inaendelea kesho kwa michezo miwili kupigwa ambapo KMC ambao watakuwa wenyeji wa Azam FC Majira ya saa Moja jioni wamesema hawatishiki na uwezo wa wapinzani wao kwani wanajiamini katika uwezo wa kupambana.

Akizungumza mara baada ya kumaliza mazoezi Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, Kocha wa KMC Fredy Felix Minziro amesema, mchezo dhidi ya Azam FC wanauchukulia kwa uzito wa hali ya juu kwani licha ya kutafuta matokeo mazuri lakini pia anaangalia uwezo wa wachezaji wake kutokana na uzoefu walionao wapinzani wao.

Hii mechi naichukulia kwa uzito mkubwa kwa sababu nawaheshimu Azam FC, ni timu kubwa na imefanya usajili zuri na hata kwenye Ligi kiwango chao ni kizuri lakini KMC ndio kwanza tumepanda kushiriki Ligi kuu kwa msimu ujao na Azam wapo kwenye Ligi kuu kwa kipindi kirefu kwahiyo mechi hii itakuwa ni kipimo tosha kwetu kuangalia kwamba uwezo wa timu yetu upo vipi, ” amesema.


Kocha Minziro amesema, ameshawahi kuwaona Azam FC mara nyingi wakicheza na hajaona tofauti ya wachezaji alionao na wale wa Azam FC japo wapinzani wao wanawachezaji wa Kimataifa na wenye uwezo lakini hawezi kuhofia huku akiongeza kuwa kufanya vizuri kwenye ASFC ni chachu au mafanikio ya kupanda kushiriki Ligi kuu msimu ujao ndio umewapa nguvu ya kuweza kufanya vizuri kwenye FA.


Nawaamini sana vijana wangu a sioni tofauti na wale wa Azam FC japo wanawachezaji wa Kimataifa na wenye uwezo lakini bado sina hofu nao na naimani kubwa sana na vijana wangu hivyo kubw ani kuwaomba mashabiki waweze kuja Chamazi kesho kwaajili ya kutupa sapoti kama walivyokuwa wakifanya katika mechi zilizopita naamini tutasonga mbele katika michuano hii, ” amesema.

Kwaupande wake Beki wa Timu hiyo Juma Jabu amesema, kila mchezaji anajua jukumu alilonalo katika mchezo huo na wanawaheshimu wapinzani wao japo lengo kubwa lililombele yao ni kusonga mbele katika michuano hiyo.

Muda hatuna tatizo nao kwani hakuna kuwa na jua na hali ya hewa itakuwa nzuri, kila mchezaji naamini kajipanga vizuri kwaajili ya kuweza kupambana, Azam ni timu kubwa na inawachezaji wenye uwezo mzuri lakini sisi tumejipanga kupambana na kuweza kushinda katika mchezo huo ili tusonge mbele, ” amesema.

Mbali na mchezo huo, mchezo mwingine utakaopigwa hapo kesho ni Singida United ambao watawakaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa Namfua Mjini Singida huku Mzunguko huo wa Nne(4) utaendelea tena Jumapili Februari 25, 2018 kwa Buseresere kuwaalika Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Nyamagana Mwanza mchezo utakaochezwa saa 8 mchana wakati Majimaji FC ya Ruvuma watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Majimaji kuwakaribisha Young Africans ya Dar es Salaam mchezo ukichezwa saa 10 jioni nao Ndanda FC watakuwa ugenini kucheza na JKT Tanzania Azam Complex Chamazi saa 1 usiku.

Mzunguko huwa wa 4 utakamilika Jumatatu Februari 26, 2018 Kiluvya United dhidi ya Tanzania Prisons saa 8 mchana Uwanja wa Mabatini na Stand United watawaalika Dodoma FC saa 10 jioni uwanja wa Kambarage.



           KMC katika moja ya mchezo wa Kirafiki waliokutana na Azam FC Uwanja wa Chamazi

No comments