SIMBA YAPIGA HATUA MOJA KUELEKEA GOODISON PARK


Mabingwa wa Tanzania timu ya Simba imepiga hatua moja kwenda kucheza na Everton ya Uingereza baada ya kuingia fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup.

Bingwa wa michuano hiyo atakwenda kucheza na Everton katika uwanja wa Godson Park ambao wamemtangaza kocha Marco Silva kuwa meneja wao mpya akichukua mikoba ya Sam Alladyce.

Simba imefika hatua hiyo baada ya kuifunga Kakamega Homeboyz kwa mikwaju ya penati 5-4.

Simba iliingia katika mchezo huo bila ya kocha wao mkuu Mfaransa Pierre Lechantre ambaye alikaa jukwaani huku sababu ya kufanya hivyo ikiwa haijatolewa ambapo msaidizi wake Masoud Djuma akiwaongoza Wekundu hao.

Wekundu hao leo walicheza vizuri kuliko mchezo wa kwanza walioshinda kwa penati pia dhidi ya Kariobangi Sharks.

Penati za Simba zilifungwa na Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya na Jonas Mkude wakiwa hawajakosa hata moja.

Baada ya mchezo huo wachezaji wa Simba walikwenda kushangilia na kocha Masoud wakionyesha hali ya kumuunga mkono baada ya kuachiwa majukumu ya kuwaongoza.

Mchezo wa fainali ya michuano hiyo utapigwa siku ya Jumapili saa 9 alasiri.

No comments