MEXIME NAYE TUMUITAJE?
KATIKA mchezo mmoja wa Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga,
Uwanja wa Jamhuri Morogoro, ilishuhudia Yanga wakipoteza mchezo kwa
kufungwa mabao 3-0.
Mabao ya Mtibwa Sugar yalifungwa na Dickson Daud aliyefunga moja, mengine mawili yakifungwa na Hussein Javu.
Yanga
iliyokuwa inafundishwa na Mbrazil Marcio Maximo ilitoka uwanjani kichwa
chini, huku Mtibwa Sugar waliokuwa wananolewa na mzawa Meck Mexime
wakitoka kifua mbele.
Baada ya mechi kuisha kundi kubwa la Waandishi lilikwenda kusimama mbele ya Mexime na kutaka maoni yake juu ya mchezo.
Katika
dharau ziliyoje Mexime alisema wao makocha wazawa hawapewi heshima
stahiki kutokana na uzawa wao, lakini wao makocha wazawa wanaweza
kuwasumbua makocha wa kigeni.
Mexime
aliongeza kuwa hawezi kufungwa kiurahisi na makocha wa kizungu na
kueleza kuwa makocha wa kizawa wanapaswa kuheshimiwa na si kupuuzwa.
Huyu ndiye Mexime ambaye hakuwa na cha kupoteza jioni ile.
Hapa
waandishi ilibidi wabaki kuwa wasikilizaji zaidi kuliko wahoji maswali.
Mexime na Mtibwa Sugar yake wameifunga Yanga idadi kubwa ya mabao,
unadhani ungemzuia asizungumze kile anachojisikia? Ingekuwa ngumu
kumzuia!
Kutoka pambano
lile la Jamhuri Morogoro, mpaka leo mambo mengi yamebadirika kwa kasi
kubwa, Mexime si kocha wa Mtibwa Sugar wala Maximo si kocha wa Yanga.
Leo hii Mexime amekuwa kocha wa Kagera Sugar na Maximo amerudi kwao Brazil. Kila mmoja yuko kivyake.
Imetuchukua muda mrefu sasa kumuona Mexime akiwa na hali mbaya ndani ya Kagera Sugar. Anatia huruma!
Ukisikiliza
majibu yake katika mahojiano na watangazaji wa vipindi vya michezo siku
hizi, unaona kabisa pole pole Mexime ameanza kumeza matapishi yake.
Amekuwa
Mexime mkali, anayetoa majibu ya hovyo tofauti na kuzungumza kiufundi
zaidi nini kimeipata Kagera Sugar yake kuwa katika sura hii.
Kuna somo la bure hapa tunapaswa kulipata kutoka kwa Mexime aliyeshindwa kuwaheshimu makocha wenzie wakati ule.
Zamani kidogo niliwahi kuiona interview ya kocha wa Aston Villa Martin Oneil, akizungumzia mchezo wao dhidi ya Arsenal.
Katika
utulivu wa hali ya juu kabisa Oneil alisema wanaiheshimu Arsenal na
wanamuheshimu Wenger na kuongeza kuwa wamejipanga kushinda dhidi ya
Arsenal.
Walivyokwenda
uwanjani Aston Villa walienda kushinda mechi, bado Oneil alitoka mbeke
ya waandishi wa habari na kuwaambia kuwa wametumia udhaifu wa Arsenal
kushinda mechi.
Oneil hakuwa na maneno mengi. Alivyomaliza kusema hivyo aliinuka katika kiti cha mahojiano na kuondoka.
Muda huu ambao Mexime anajipapatua kuirudisha upya Kagera Sugar, nae tumuite jina gani.
ABDUL MKEYENGE
Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza
kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.
Post a Comment