JOHN GEORGE TIBER, REMEMBER THIS NAME
ABDULAH MKEYENGE
ACHANA na Mrisho Ngassa. Achana na Jabir Aziz ‘Stima’, Achana na Nassor Kapama. Achana na Malale Hamsini na msaidizi wake Mussa Mbaya ‘Molloto’, Ndanda FC ina kijana mmoja anayeitwa John George Tiber. Achana na kijana huyu. Tiber ni dhahabu. Tiber ni promissing player.
Katika timu ya Ndanda FC ambayo haina uhakika wa kulipa mishahara wachezaji wake, leo nasimama hapa kwa kutumia kalamu yangu na kujiaminisha kuwa Tiber atakuwa mchezaji wa kwanza kikosini humo kusajiliwa timu nyingine na kupata uhakika kulipwa mshahara wake. Kila nikimtazama Tiber naamini hivi. Siamini vingine.
Kinachoniamisha ni kitu kimoja tu. Ubora wake. Ana ubora mkubwa. Ni miongoni mwa wachezaji wanaorahisisha mpira tuliowashuhudia msimu huu. Sehemu ya kutembea na mpira anatembea nao, sehemu ya ku’shoot ana shoot, sehemu ya kutoa pasi anatoa, sehemu ya kufunga bao anafanya hivyo. Rejea bao lake dhidi ya Mwadui FC wiki iliyopita. Aliwafanya alivyotaka wachezaji wa Mwadui FC, kisha akafunga bao la kideo.
Mambo yote haya anayafanya akiwa katika kasi. Ni wachezaji wachache wanaofanya mambo hayo wakiwa na kasi, wengi wanakosa kasi. Rafiki yangu Ibrahim Ajib ni fundi wa mpira kweli kweli, lakini hana kasi aliyonayo Tiber. Kuna wakati unashangaa na kujiuliza, inakuwaje Geofrey Mwashiuya anachezea Yanga, Tiber Ndanda FC?
Msimu wake wa kwanza katika ligi ameutendea haki. Utulivu wake akiwa na mpira miguuni huwezi kuamini kama ni kijana mdogo mwenye miaka 19. Amekuwa na maendeleo mazuri kwa kiwango chake. Ukiingia uwanjani kuitazama Ndanda FC, ukiwa humjui Tiber, ni rahisi kumjua kutokana na ubora wake. Nasikia timu nyingi zimeshaanza kupiga hodi kuitaka saini yake akajiunge nazo. Nilijua tu!
Namuona mbali kijana huyu kama ataendelea kuwa hivi alivyo. Vijana wengi wanaanza na kasi hii kama aliyonayo Tiber, lakini wakifika muda wa kuwa wachezaji timilifu wanageuka wachezaji wa kawaida wanaouogopa mpira. Zlatan Naldo ni mmoja wao.
Naldo ni kijana mmoja wa mtaani kwangu aliyekuwa anakuja vizuri na kutufanya mtaa mzima tuamini kupitia yeye atatutambulisha vyema, lakini muda aliotakiwa kukomaa na kufika mbali akageuka mchezaji wa kawaida anayeogopa hata kupasiwa mpira na wenzie.
Namuombea Tiber safari njema. Natamani sana kuona mwisho wa kipaji chake hiki anachotunoyesha leo akiwa na miaka 19 tu. Kama atakuwa na mwendelezo mzuri akifikisha miaka 23, Tiber atakuwa amemfuata ulaya Mbwana Samatta bila wasiwasi wowote ule.
Kuna sehemu wachezaji wetu wanafeli. Usimamizi ni sehemu nyingine inayowafanya wakose miendelezo ya vipaji vyao na baada ya miaka kadhaa kupita inabaki kuwa historia kuwa kuna mchezaji alikuwa akiitwa John George Tiber, lakini alishindwa kuendelea na soka kutokana na nidhamu yake. Mitaani tuna wachezaji wengi wa namna hii.
Tiber anapaswa kuinamisha chini shingo yake na awaze mpira, alale mpira, atembee mpira, ale mpira na avae mpira. Ni ngumu kufanikiwa kama atauchanganya mpira na mambo yake mengine.
Akiufanya mpira kama mtaji wake kupata mafanikio atafika nchi ya ahadi ambayo wachezaji wenzake wengi wameshindwa kuifikia nchi hiyo, lakini akiufanya mpira kama sehemu yake ya burudani, ajue kabisa baada ya muda mfupi ataishia kuwa mchezaji wa timu za maskani. Kuna mifano mingi ambayo Tiber anapaswa kuitumia ili iweze kumuongoza.
Mwisho kabisa msomaji wangu nikutajie tena jina hili John George Tiber, remember this name. Liweke akilini mwako jina hili, kuna siku litakuja kutikisa soka letu. Wait and see!
Post a Comment