INFANTINO,AHMAD WAMEINGIA NCHINI NA KUKUTANA NA PINGAMIZI LA FDL , NANI APANDE VPL
RAIS wa FIFA Gianni Infantino yuko
nchini. Rais wa CAF Ahmad Ahmad nae yuko nchini. Kamera za ulimwengu wa soka
zinaimurika Tanzania katika lenzi mbonyeo na mbinuko.
Infantino, Ahmad wameingia nchini
asubuhi ya leo wakilakiwa vizuri na wenyeji wao Waziri wa Habari, Tamaduni
Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa BMT Leodegar Tenga na
Rais wa TFF, Wallace Karia. Ni ujumbe mzito uliowapokea marais hao wa FIFA na
CAF.
Marais hao wamekuja Tanzania muda
ambao raia wake wanataka kuona soka la nchi likifika nchi ya ahadi.
Harakati za kufika nchi ya ahadi
hazijaanza juzi, jana wala leo, zilianza siku nyingi tu, lakini zilikosa
mwongozo wenye mtazamo chanya.
Ni kama tumesimama sehemu baada ya
mafanikio yetu ya mwaka 1980 pale Lagos tulipofuzu kucheza Mataifa Afrika kwa
mara ya kwanza na ya mwisho. Tangu hapo tumeweka kituo kwa kusimama, hatujafuzu
tena mpaka leo.
Nini shida? Wapi tulipokwama? Nani
hawajibiki? Maswali yote hayo yanakuja na majibu ya kitu kimoja kinachoitwa
Serikali.
Serikali ndiyo wenye majibu ya
anguko la soka letu na rafiki zangu wa TFF wao wanabeba sehemu ndogo ya lawama
za soka la nchi kusimama.
Lawama za TFF ni kama hivi, Daraja
la kwanza (FDL ) imeisha wenyewe hawajazithibitisha timu zilizopanda, badala
yake wanasubiri kupitia pingamizi. Kuna timu zimekatiwa rufaa.
Matatizo ya TFF ndiyo haya. Hivi
bado tunaishi dunia ya kukata rufaa kwa maana ya kupinga matokeo ya
uwanjani?
Ina maana timu iliyoshinda uwanjani
inaweza isipate nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara na timu itakayoshinda mezani
ndiyo ipate nafasi hiyo? Kila leo tunapiga hatua za kurudi nyuma, sio mbele.
Muda huu ambao Infantino, Ahmad wako
nchini timu zilizopanda daraja zilipaswa kushangilia, kujiandaa na ushiriki wao
wa ligi msimu ujao, lakini badala yake timu hizo zimemaliza ligi uwanjani sasa
zimehamia ligi ya mezani. Jamani wapi tunaupeleka huu mpira?
Kinachoonekana hapa kwa yaliyotokea
miaka miwili iliyopita yanaweza kutokea na mwaka huu. Kuna kula dalili hiyo.
Miaka miwili iliyopita tulishuhudia Mbao FC ikipandishwa daraja, huku Geita na
timu nyingine zikishushwa. Hili linaweza kutokea na mwaka huu. Dalili ziko
wazi.
Mpaka tumefikia hatua ya kujiwa na
watu wazito kama Ahmad, Infantino, tunapaswa kubadilika jinsi ya uendeshaji
soka. Kama wageni hao wakihadithiwa stori hii wanaweza kutupuuza ghafla.
Kwanini tupuuzwe katika jambo la kipuuzi?
Tuikatae aibu hii. Tena tuikatae na
kuipinga kwa nguvu kubwa kama klabu za ulaya wanavyopinga dhambi ya ubaguzi wa
rangi kwa kiasi kikubwa.
Infantino, Ahmad karibuni, lakini
haya ndiyo maisha yetu, ila rai yetu mkirudi makwenu msiende kuwaambia haya.
Post a Comment