SERIKALI, TFF YAENDELEA NA MAANDALIZI UGENI FIFA, WAGENI TAKRIBANI YA 70 KUHUDHURIA MKUTANO WA FEBRUARI 22

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Harrison mwakyembe amesema, wapo katika maandalizi ya mwisho kwaajili ya mapokezi ya Viongozi watakaohudhuria Mkutano wa FIFA utakaoshirikisha nchi 19 wanachama wa FIFA utakaofanyika Februari 22 Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.

Akizungumza na wahariri wa Habari za Michezo, Waziri Mwakyembe ameendelea kusisitiza suala la ukarimu kwa wageni hao ambao wanatarajiwa kufikia idadi ya wajumbe 70 huku akiongeza kuwa anaamini Mkutano huo pia utasadia kuleta maendeleo ya soka hapa nchini.

"Baadhi ya wageni wameshaanza kuwasili leo, na wajumbe wataanza kuwasili Februari 21, tunatarajia kuwa wageni takribani 70 hapa nchini ambao watahudhuria mkutano huo utakaofanyika Februari 22, Rais wa FIFA atawasili siku moja kabla ya mkutano na mimi nitamfuata hotelini kwaajili ya kwenda naye Ikulu kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, " amesema.



"Niendelee kuomba tuu ukarimu kwani ugeni huu ni mzito sana na ni kwa maendeleo ya soka letu hapa nchini hivyo naamini mara baada ya kutano huo, kutakuwa na fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari hivyo naamini tutakuwa na ushirikiano nao mzuri, " amesema.



Kwaupande wake Katibu Mkuu wa TFF Wilfedy Kidau amesema, katika Mkutano huo ambao utaongozwa na rais wa FIFA Gian Infantino Tanzania imepata bahati ya kuwakilisha wajumbe watatu pamoja na kuwasilisha masuala ya soka la vijana.



"Ajenda za mkutano italenga katika miradi mbalimbali ya Fifa zamani ikifahamika kama Goal Project na sasa ikifahamika Fifa Forward Programme,ajenda ya soka la vijana,Wanawake na klabu wakati ajenda nyingine ya mkutano huo ni kujadili kalenda ya kimataifa ya Fifa,kuboresha masuala ya uhamisho na vipaumbele vyake , kwa upande wetu Tanzania tumepata bahati ya kushiriki wajumbe watatu ambapo atakuwa Rais wa TFF, katibu Mkuu ambaye ni mimi pamoja na Leodgar Tenga akiwa ni Rais wa Heshima wa TFF, " amesema.



Kidau amesema, wamejiandaa vizuri kwaajili ya kupokea ugeni huo kutoka nchi za Bahrain,Palestina,Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu(UAE),Algeria,Burundi,Africa ya Kati,Ivory Coast,Mali,Morocco,Niger,Tunisia,Bermuda,Monserrat,St,Lucia,Us Virgin,Maldives na Congo.
                                                    
                                   Waziri wa Michezo Mheshimiwa Harrison mwakyembe

No comments