USHINDI DHIDI YA GENDARMERIE HAINA MAANA KWAMBA TUMEVUKA, TUNAKAZI NGUMU DJIBOUT - SIMBA SC

Mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Gendarmerie Tnale hapo jana katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, Uongozi wa Klabu ya Simba umesema ushindi huo haumaanishi kwamba wameshavuka katika hatua hiyo kwani mchezo wa marudiano ni mgumu na unahitaji taahadhari kubwa.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya Simba SC Haji Manara amesema, bado hawajafuzu kwa mzunguko unaofuata bali wameshinda mchezo wa dakika 90 hivyo bado 90 zilizobakia na hata wapinzani wao ni timu nzuri ambayo inaonyesha wanaweza kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Februari 20 nchini Djibout.


Bado mechi haijaisha, hatujafuzu bado kwa mzunguko unaofuata kwasababu mechi hizo ni dakika 180 nyumbani na ugenini, mechi ya nyumbani tumeshinda bado ya ugenini, kwahiyo tunaangalia mechi ya ugenini itakayochezwa Djibout, ” amesema.

Manara amesema, timu waliyokutana nayo ni nzuri na yenye kucheza kwa kuheshimu mchezo na wanaamini wanaweza wakaona mchezo mzuri zaidi wa wapinzani wao zaidi ya ule walioucheza hapo jana.

Sio timu mbaya kama watu wengi wanavyodhani na jana tumeona, wanacheza kwa kuzia sana na wamejitahidi, bila shaka wanaweza wakafunguka wakiwa kwao na hapo tunaweza tukaona mchezo mzuri zaidi kuliko tuliouona jana, ” amesema.

Wakati huoho Manara ameongeza kuwa, Kikosi kamili cha wachezaji wa Klabu ya Simba kinatarajia kuondoka kesho kuelekea Mjini Shinyanga kwaajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Mwadui FC utakaopigwa Alhamisi ya wiki hii huku wakimkosa beki wao Mghana ambaye anamiliki kadi tatu za njano pamoja na wachezaji ambao bado ni majeruhi ndani ya kikosi hicho.

Tunakwenda na Kikosi kamili Shinyanga, tunatarajia kumkosa Asante Kwasi kwasababu anakadi tatu za njano, pia wachezaji waliokuwa na majeraha ya muda mrefu ambao sasa wameshaanza kufanya mazoezi, lakini tukirudi kutoka Shinyanga tutataja timu kamili itakayoondoka kuelekea Djbout lakini bila shaka tutaondoka na timu yote kwa sababu unajua ratiba ni ngumu kwahiyo tukitoka Djibout tunakutana na mechi ya Ligi hapa na Mbao kwahiyo hatuwezi kuwaacha wachezaji katika safari ya Djibout, ” amesema.

Simba SC ilipata ushindi wa bao nne kupitia kwa kiungo Said Hamisi Ndemla, Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco aliyefunga magoli mawili na mshasmbulaiji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi.

No comments