YANGA YAREJESHWA TENA UWANJA WA NAMFUA KWENYE ASFC
Mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara klabu ya Yanga imepangiwa
kucheza na Singida United kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe la
shirikisho nchini, mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Namfua mjini
Singida.
Robo fainali hiyo imetokana na droo iliyochezeshwa leo na wachezaji
wa zamani George Masatu aliyechezea Simba SC na Yahya Issa aliyechezea
Yanga, chini ya usimamizi wa Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Jemedari Said.
Mechi hyo itakuwa ni marudio ya mechi ya kwanza ambapo timu hizo
zilikutana kwenye uwanja huo wa Namfua kwenye raundi ya kwanza ya ligi
kuu na kutoka sare ya 1-1.
Mbali na mchezo huo mechi nyingine za robo fainali zitakuwa kati ya
Azam FC watakaokuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar, Stand United
watakaoikaribisha Njombe Mji FC na Tanzania Prisons watakaokuwa wenyeji
wa JKT Tanzania.
Safari ya Yanga katika michuano hii ilianzia kwa kuiondoa Reha FC
katika mechi ya hatua ya 64 kabla ya Yanga kusafiri hadi Mbeya na kuitoa
Ihefu katika hatua ya 32 Bora kisha ikasafiri kwenda Songea katika
hatua ya 16 Bora na kuitoa Majimaji na sasa itasafiri tena kwenda
Singida.
Mechi za Robo Fainali zitachezwa kati ya Machi 30 na Aprili 1, mwaka
huu katika viwanja vya Namfua, Singida, Azam Complex, Chamazi, Dar es
Salaam, Sokoine mjini Mbeya na CCM Kambarage, Shinyanga.
Post a Comment