Makala:Dilunga halisi amezaliwa tena Manungu


NA:ABDULAH MKEYENGE

HUWA inatokea kwenye mchezo wa soka. Na hivi karibuni ilimtokea kiungo Hassan Dilunga alivyokuwa katika jezi za Yanga, Ruvu Shooting, Stand United.

Kote huko Dilunga alikuwa hovyo, hakuwa Dilunga tuliyemzoea. Utulivu wake, umakini wake, vyote vilipotea kama jua la magharibi linavyozama.

Huyu hakuwa Dilunga tuliyemfahamu na kikosi cha JKT Ruvu Stars. Dilunga wa JKT Ruvu Stars alikuwa kila kitu uwanjani.

Ruvu Stars walicheza kwa spidi yake, ni yeye aliyekuwa anaamuru mpira apasiwe nani na kwa wakati gani. Aliing'arisha na kujing'arisha sana katika jezi za Ruvu Stars.

Samaki wakubwa wakavutiwa nae. Simba, Azam na Yanga zote zilimuhitaji, lakini walikuwa Yanga waliofanikiwa kuinasa saini yake. Akatua Jangwani na kuvua gwanda la jeshi. Ndoto zake nyingi zilianzia kufia hapa.

Ndani ya Yanga hakuwa Dilunga tuliyemzoea. Alikuwa wa tofauti mno aliyepoteza kujiamini kuanzia umiliki wa mpira hadi kupiga pasi kwa washambuliaji.

Yanga wakamuondoa, hawakupata kile walichokitaraji. Akaondoka zake kwenda Stand United, huko nako alikuwa Dilunga yule yule wa Yanga.

Akaondoka na kurudi Ruvu Shooting, huku nako alienda kuendeleza alichokuwa amekifanya Yanga na Stand United.

Mtibwa Sugar wakamsajili mwanzoni mwa msimu huu. Pole pole makocha Zubeir Katwila na Patrick Mwangata wameamza kumrudisha Dilunga wetu tuliyemzoea.

Utulivu, umakini, pasi za mwisho, ufalme kwenye eneo la kiungo vyote vimerudi tena kwenye bongo na miguu ya Dilunga, kuna biashara nzuri Mtibwa Sugar wanaweza kuifanya mwishoni mwa msimu huu. Stay tune.

Huyu tunayemtazama sasa ndiyo Dilunga halisi tuliyewahi kumtazama miaka minne iliyopita.

Tena Dilunga wa siku hizi ameongezeka kitu kipya. Amekuwa na mfungaji pia, sio Dilunga yule aliyekuwa akiuamrisha mpira pekee, Dilunga huyu anafunga pia.

Tanzania tuna viungo wachache wenye uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kufunga. Laphael Loth wa Yanga na Mzamiru Yassin wa Simba waliifanya kazi hii msimu uliopita, lakini msimu huu hawafanyi tena kazi hizo.

Muda huu ambao Mzamir na Laphael wameshindwa kukirudia kile walichokifanya msimu uliopita, wakati huu wacha tufaidi ubora wa Dilunga anayetupa vitu viwili kwa wakati mmoja uwanjani.

Nasikia Yanga wameanza kumtamani tena. Katika ubora huu wa leo si Yanga peke yao wanaotamani tena huduma ya Dilunga, ziko timu nyingi.

No comments