SINGIDA UNITED YAFURAHISHWA KUONDOKA KWA KOCHA MHOLANZI

Uongozi wa Klabu ya Singida United umesema unajisikia fahari kuona baadhi ya Vilabu vikubwa vya Soka ndani na nje ya nchi kumuhitaji Kocha wao Mholanzi, Hans van der Pluijm kwani wanaamini ni Kocha mkubwa na wenye uwezo ndio maana vilabu hivyo vimemtolea macho kuhitaji huduma yake.

Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga amesema bado wanamkataba na Kocha Hans lakini iwapo utafika wakati wa kuondoka hawawezi kumzuia kwani ni kazi yake na hawatakuwa na tatizo na Klabu yoyote itakayomuhitaji.

“Sisi tunaona ni fahari, unajua ukiona Klabu ndogo lakini ni kubwa kwamaana imeingia kwenye Ligi kuu msimu huu na inakocha mkubwa kama Hans na vilabu vikubwa vinamuhitaji, kwanza tumepokea ofa nyingi kutoka Marekani, na pia kuna Klabu kutoka Sudan wakimuhitaji lakini vipo vilabu vikubwa hapa nchini vinamuhitaji, sisi ni heshima kwetu kwamba ni moja kati ya Klabu ambayo vilabu vikubwa vinaweza kuiangalia na kumuhitaji Kocha, ” amesema.

“Sisi Hans bado tunamkataba naye lakini tunaamini kabisa anaweza kuondoka kwasababu hivi vilabu vimekuwa na nguvu kubwa sana ya kumuhitaji, lakini Hans bado anamapenzi na Singida United, ila sisi hatuwezi kumzuia kwasababu yeye pia anatafuta riziki kupitia kazi yake, kwahiyo kikubwa ni kwamba Hans kwa sasa anayemuhitaji sisi hatuna tatizo, ” amesema.

Sanga ameongeza kuwa kuelekea katika muendelezo wa Ligi kuu wakiwa wamebakisha mechi tano ambapo kesho watakuwa ugenini wakipambana na Mbeya City kikosi kimejipanga kuhakikisha kinaendelea kulinda heshima ya Timu na pia kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kusalia katika nafasi za juu mwishoni mwa msimu wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

“Tunapambana ili kwenye Ligi kuu historia yetu iweze kubaki kuwa salama kwamaana tunahitaji kuwa kwenye nafasi nne, tatu au mbili na hilo linawezekana kwasababu mpira unadunda na bado tunamechi tano kabla ya kumaliza Ligi kwahiyo hauwezi jua kitakachotokea, ” amesema.

“Tunaenda kucheza na Mbeya City tukiwa tunawaheshimu kwani wametoka sate na timu kubwa kama Yanga hivyo naamini hata sisi wametupania na pia wanahitaji kujiondoa katika nafasi waliyopo, lakini sisi sio ngazi ya wengine kung'ang'ania kutokushuka daraja, sisi tunacheza mpira na hatuingii Uwanjani kumpa mpinzani wetu pointi tatu bali tunapambana, ” amesema.
Kocha wa Singida United,, Hans van der Pluijm

No comments