KAHEZA AAHIDI MAKUBWA BAADA YA KUTUA SIMBA


Mchezaji mpya wa timu ya Simba aliyesajiliwa kutoka Majimaji, Marcel Kaheza ameahidi kufanya vizuri akiwa na mabingwa hao wa VPL msimu ujao.

Kaheza amekuwa na msimu mzuri akiwa na Majimaji akifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa ligi wa mwezi Aprili kitu kilichowavutia Simba kumsajili.

Mshambuliaji huyo aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Simba miaka kadhaa iliyopita na kushindwa kufanya vizuri kutokana na kukutana na wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi yake.

Kaheza alisema anaamini safari hii amerejea Simba akiwa mtu mzima hivyo atapigania namba kutokana na kikosi cha Wekundu kusheheni nyota wenye uwezo wengi mkubwa.

"Nimerejea Simba kwa mara nyingine nikiwa na mtu mzima, nawaahidi mashabiki na wapenzi wa Simba mambo mazuri kutoka kwangu kuanzia msimu ujao," alisema Kaheza.

Kaheza ataichezea timu yake ya Majimaji leo mechi ya mwisho dhidi ya timu yake mpya ya Simba katika mchezo wa kufungia msimu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea saa 10 jioni.

No comments