DILUNGA AFUNGUKA SIRI YA MAFANIKIO YAKE MTIBWA
Mchezaji bora wa michuano ya Azam Sports Federation Cup, Hassan Dilunga amesema mshikamano ndani ya kikosi cha Mtibwa Sugar ndio siri ya mafanikio yake msimu huu.
Dilunga amekuwa na msimu mzuri na kuchangia kiasi kikubwa katika ubingwa wa FA iliyopata Mtibwa jana kwa kuifunga Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali.
Nyota huyo wa zamani wa timu za Yanga na Ruvu Shooting amesema kujituma, uvumilivu na kusikiliza mafunzo kutoka kwa walimu pamoja na mshikamano ndani ya kikosi ndicho kilichomfikisha hatua hiyo.
"Unajua kikubwa ni kujituma, kumsikiliza mwalimu, mshikamano na kutambua unatakiwa kufanya nini na wakati gani ndio silaha kubwa iliyonifikisha hapa," alisema Dilunga.
Kiungo huyo ameifungia Mtibwa mabao muhimu msimu uliomalizika kuanzia kwenye ligi hadi kombe la FA.
Dilunga anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoiongoza Mtibwa katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Post a Comment