MANULA HATIHATI KUIKOSA KAKAMEGA KESHO
Mlinda mlango namba moja wa timu ya Simba, Aishi Manula huenda akakosa mchezo wa kesho wa nusu fainali wa SportPesa Super Cup dhidi ya Kakamega Homeboyz kutokana na kupata maumivu ya mguu.
Manula alipata maumivu katika mchezo uliopita dhidi ya Kariobangi Sharks ingawa alimaliza dakika zote 90 na kwenda katika hatua ya makundi.
Mkuu wa kitengo cha habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Manara ambaye yupo nchini Kenya na kikosi hicho amesema watasubiri taarifa ya daktari kesho ili kujua kama atacheza au la kwakua alipata maumivu katika mchezo uliopita.
"Kikosi kipo vizuri isipokuwa Manula tutasubiri kwanza vipimo vya daktari kama atakuwa sehemu ya mchezo ingawa hajapata maumivu makubwa," alisema Manara.
Mchezo huo utaanza saa 7 mchana katika uwanja wa Afraha ukifuatiwa na nusu fainali ya pili kati ya Gor Mahia dhidi ya Singida United saa 9 alasiri.
Post a Comment