SIMBA, YANGA KUKUTANA MWEZI UJAO TAIFA


Timu za Simba na Yanga zitakutana katika michuano ya Cecafa Kagame Cup itakayoanza Juni 28 hadi Julai 13 baada ya kupangwa kundi C.

Miamba hiyo ya soka nchini itakutana katika mchezo huo ambao utafanyika Julai 5 katika uwanja wa Taifa saa 12 jioni.

Wababe hao Dar es Salaam wamepangwa kundi moja pamoja na timu za St. George ya Ethiopia  na Dakadaha ya Somalia.

Kwa upande wa mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC wamepangwa kundi A pamoja na JKU ya Zanzibar, Uganda Reps ya Uganda pamoja na Kator FC ya Sudan Kusini.

Kundi B itakuwa na timu za Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi pamoja na Ports ya Djibouti.

Michuano hiyo itachezwa katika viwanja viwili ambavyo ni Azam Complex na Uwanja wa Taifa.

Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amesema wanaamini michuano itakuwa mizuri kutokana Tanzania kuwa na historia nzuri kila inapoandaa.

"Michuano ya Cecafa itaanza Juni 28 mpaka Julai 13 na itashirikisha timu 12 kutoka katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na Kati," alisema Musonye.

Michuano hiyo itarushwa moja kwa moja na Azam TV ambapo Mkurugenzi wake Tido Mhando amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha inakuwa bora na ya kuvutia.

No comments