GENNARO GATTUSO KATIKA UBORA WAKE NDANI YA AC MILAN.



SIKU moja katika viwanja vya mazoezi AC Milan, Gennaro Ivan Rino Gattuso aliyesimama hatua chache alikokuwa Andrea Pirlo, alimfuata na kumwambia hajioni kama anastahili kuitwa mchezaji, ila Pirlo anastahili kuitwa jina hilo. 


Gattuso alimwambia Pilro kila akimtazama anajiona yeye angefaa kufanya shughuli nyingine, lakini sio kucheza soka.

Hatimaye wawili hawa wametundika daruga. Pirlo anaenda kustahafu mwishoni mwa msimu huu, Gattuso amekuwa kocha wa AC Milan klabu aliyochezea kwa mafanikio. 

Aliwahi kusema mwanafalsafa wa Kijerumani Kahl Henrik Max kuwa nyakati ngumu hupita, lakini watu wagumu hawapiti. 

Gattuso ni mtu mgumu aliyerudi uwanjani. Wakati huu akirudi  kama kocha, si mchezaji tena. Amerudi kibabe kama alivyoondoka kibabe. 

 Wakati anatangaza kung'atuka Jiji la Milan na kuungana na familia yake alitoa machozi kama ya Simba aliyefiwa na mtotowe. Hakuna aliyeona wala kujali thamani ya machozi yake zaidi ya moyo wake wa chuma uliomwagiwa damu za kikatili za Kiitaliano. 

Max alipowasema watu wagumu hawapiti alimaanisha watu aina ya Gattuso. Hawa ni watu wachache wenye mioyo ya ubondia, lakini waliamua kubeba njumu na kuja uwanjani kucheza soka.

Gattuso mtemi, mgomvi, katili asiye na chembe za huruma ndiyo kocha wa AC Milan hivi sasa. Ameichukua timu katika mazingira magumu na mwenyewe akisema anataka kurudisha heshima yao ndani ya Italy na ulaya kiujumla.

Kando ya mbinu zake kuwafikia wachezaji na wachezaji kuzitekeleza kifasaha, moyo wake mgumu umeanza kuwaingia wachezaji. 

Milan inapambana siku hizi. Wachezaji wanacheza kwa moyo mmoja. Wanacheza kana kwamba hawachezi tena mechi nyingine. 

AC Milan ya mwisho kuwa na passion hii ni ile ya kocha Massimiliano Allegri, lakini AC Milan nyingine hazikuwa zikijua thamani na uzito wa jezi wanaovaa na timu wanayochezea. 

Wiki iliyopita Gattuso na vijana wake walienda uwanja wa Stadio Olympic kucheza dhidi ya AS Roma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mpira mmoja wa kurusha beki wa Roma 
Aleksandar Kolarov alikutana na domo chafu la Gattuso.

Kolarov ameeleza kuchukizwa na kauli chafu zilizotolewa na Gattuso juu yake.

Kolarov amesema kuwa wakati akijiandaa kurusha mpira dakika ya 35 kipindi cha kwanza alibughuziwa na Gattuso kwa maneno ya kejeli ambayo hakutarajia maneno kama hayo kutoka kwenye kinywa cha Gattuso.

"Alinifuata huku akiniambia kuwa nina bahati sikucheza soka kipindi ambacho yeye alikuwa uwanjani, kwa maana kipindi chake hakukuwa na warembo kama mimi wenye maumbile ya kuvutia na kutia hamasa"
alisema Kolarov.

Nimeshangaa kitu hapa. Gattuso anatuambia Kolarov ni kama mwanamke mrembo anayeweza kumvutia mwanaume kama yeye, hapa alimzungumzia Kolarov yupi, yule aliyewahi kupita Manchester City au yupi?

Kolarov mbishi kimtazamo, kiugumu na mwenye madhara langoni mwa adui,  Gattuso alimaanisha Kolarov yupi? 

Kama ugumu wote ule wa Kolarov bado Gattuso anataka kutuaminisha anachokiamini kuhusu Kolarov, vipi siku timu yake ikicheza dhidi ya Neymar? 

Gattuso hakumfanyia fair Kolarov. Lakini shida ya Gattuso mwenyewe hajali, mara zote ni mtu wa kusema anachokiamini. Muda huu tunaotumia kuitafakari kauli yake ya kijinga kabisa, tufahamu kuwa Gattuso ndiyo yuko hivi. Alianza kutuonyesha ujinga wake wakati anacheza, wacha leo hii aendelee kutuonyesha wakati akifundisha

No comments