HESABU KALI ZA YANGA KUANZA KUONEKANA HII LEO DHIDI YA WANAKURUKUMBI KAGERA SUKARI.
MASTAA wa Yanga wakiongozwa na Papy Kabamba Tshishimbi na Obrey Chirwa,
wamepewa mpango mzima wa kuamua hatma ya Sh1.5 bilioni ambazo timu hiyo inaweza
kupata endapo itaitoa Township Rollers ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Yanga ilifungwa nyumbani mabao 2-1 hivyo inahitaji ushindi wa mabao
mawili ama zaidi ili kusonga mbele. Hata hivyo, kutokana na hali ngumu ya
kifedha inayoikabili klabu hiyo, nyota wake wakiongozwa na Tshishimbi na Chirwa
waliong’ara kwenye mchezo wa kwanza, wanalazimika kuongeza nguvu ili wavute
mabilioni hayo.
Yanga itavuna mkwanja huo kama itafuzu hatua inayofuata ya
mashindano hayo, ambapo zinatokana na fedha ambazo Shirikisho la Soka la Afrika
(CAF) hutoa kwa kila timu inayofuzu hatua ya makundi sambamba na fungu
itakalopata kutoka kwa wadhamini wake wakuu, SpotiPesa.
Lakini, kama ulikuwa
hufahamu ni kwamba ukiingia tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
unakuwa umejihakikishia kuvuna dola za Marekani 550,000 (Sh1.2 bilioni) na
kiwango hicho kinapanda kulingana na nafasi unayomaliza kwenye kundi lako.
Fedha hizo zitatiwa chachu zaidi na fungu la Sh 250 milioni linalotolewa na SpotiPesa
ikiwa ni sehemu ya makubaliano kwenye mkataba wa udhamini baina yake na Yanga.
Katika kuhamasisha zaidi mastaa wa mabingwa hao wa Jangwani kupambana ili
kupata matokeo yatayowavusha hatua inayofuata, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface
Mkwasa amesema wakifanikiwa kufuzu makundi, sehemu ya fedha hizo zitakuwa
zawadi kwa wachezaji. “Litakuwa ni jambo la ajabu mtu ukapata fedha kama hizo
halafu ukashindwa kuwapatia wale waliochangia kufanikisha hilo.
Hivyo, uongozi
tumepanga kufanya hivyo,” alisema. “Hata hivyo, hatuwezi kutangaza ni kiasi
gani hasa ambacho tutawapatia katika fungu hilo ili tusije kuwavuruga
wakapoteza utulivu kwa sababu suala la fedha ni nyeti.
Kimsingi ijulikane wazi
tu kwamba tukifuzu, basi wachezaji watanufaika.” KAGERA ANAKUFA Wakati huo huo,
Yanga itakuwa nyumbani leo Ijumaa kuumana na Kagera Sugar ikiwa ni mwendelezo
wa Ligi Kuu Bara, lakini mabingwa hao watetezi watawakosa wachezaji wake
wawili. Kikosi cha Yanga chini ya kocha, George Lwandamina kinarudi katika ligi
kujaribu kufuta majonzi ya kipigo cha mabao 2-1 walichopata kutoka kwa Rollers.
Yanga ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo, itataka kulinda heshima yake
mbele ya Kagera Sugar, baada ya kuichapa mabao 2-0 kwao Kaitaba katika mzunguko
wa kwanza, ingawa mabingwa hao watawakosa kiungo Raphael Daud na winga Geofrey
Mwashiuya wenye kadi tatu za njano.
Akizungumzia mchezo huo, Lwandamina alisema
wanarudi kupambana kusaka pointi tatu ingawa wanajua kwamba, Kagera imeanza
kubadilika kwa kupata ushindi katika mechi zake.
“Kwetu siku zote tunaipa
heshima kubwa kila timu, Kagera hawakuwa na matokeo mazuri lakini hivi karibuni
wamebadilika, mchezo wa kesho (leo) hautakuwa rahisi ila tumejiandaa
kupambana,” alisema. Kwa upande wake, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime,
alisema hata kama Yanga imetoka kupata kipigo katika mchezo wa kimataifa,
wanapokutana Bara ni mechi tofauti na kila timu inapambana kusaka ushindi.
“Tumekuja kutafuta ushindi, hilo suala la Yanga kupoteza hiyo ni mechi tofauti,
nashukuru kila kitu kipo sawa kwa upande wetu, sina majeruhi tunachotaka ni
pointi tatu,” alisema Maxime.
Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.
Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.
Post a Comment