OKWI AJITABIRIA IDADI YA MAGOLI ATAKAYOWAFUNGA WAARABU UGENINI NCHINI MISRI.


STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi, amewatuliza mabosi na mashabiki wa timu hiyo akiwaambia wasiwe na presha ya marudiano na Al Masry kwani anakwenda kupiga mabao ya kutosha. Amechimba mkwara kuwa anazifahamu mbinu zote za mabeki wa Al Masry hivyo, ni lazima atawafunga tu kwao.


Simba ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Al Masry juzi Jumatano usiku katika Kombe la Shirikisho, lakini staa huyo amesema nafasi yao kusonga mbele bado ni kubwa.

Okwi, aliyeifungia Simba mabao 19 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu, alisema beki ya Al Masry inapitika na kwenye mchezo wa marudiano atakuwa fiti zaidi hivyo, hawataweza kumzuia. Mganda huyo alisema anajua watakapokuwa kwao watafunguka zaidi na hapo ndipo atakapowamaliza kiulaini.

Nyota huyo aliyewahi pia kuzichezea Yanga, Etoile ya Tunisia na Sondersjske ya Sweden, alisema kwa sasa wanapambana kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini tayari akili ameshaiweka sawa katika mchezo wa marudiano.

“Walikuwa wengi katika ukuta wao (juzi) tulipambana kuwafungua na kufanikiwa kwa kiasi hicho, lakini sasa nimewajua vyema mabeki wao,” alisema Okwi. “Kule kwao najua watafunguka na hicho ndiyo ninachokitaka, nitawafunga wala sina wasiwasi.

Najua makocha wameona udhaifu wao na ubora wao, wala Wana Simba wasiwe na shaka.” MIKAKATI KIBAO Kutokana na uzito wa mchezo wa marudiano, viongozi wa Simba wameanza kuandaa mikakati ya ndani na nje ya uwanja ili kwenda kuwang’oa Waarabu hao kwenye ardhi yao.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema wamejifunza kuhusu figisu za nje ya uwanja, hivyo hakuna wanalolihofia. “Simba tumeamka na tupo tayari kupambana na figisu zote za nje ya uwanja huko, miaka ya nyuma ndio walikuwa wanatuvuruga sio sasa,” alisema “Tutaifunga Al Masry kwao, kama viongozi tayari tulishaanza kuandaa mikakati ya ndani na nje.”

LECHANTRE NAYE Kocha Pierre Lechantre alisema kama kuna siku vijana wake walimfurahisha basi ni katika mchezo wa juzi na sasa anataka kutulia na kufanya mambo mawili yatakayowapa matokeo mazuri ugenini. Alisema mchezo wa ugenini utakuwa na sura tofauti ya ugumu hivyo, wanahitaji muda mwingi wa kujiandaa.

Mfaransa huyo alisema anaiheshimu Al Masry, lakini endapo watafanya maandalizi ya kutosha basi ana nafasi ya kuwang’oa Waarabu hao. “Vijana wamenifurahisha, nafikiri kwa mara ya kwanza wamefanya kile ninachokitaka kiwe katika timu ninayoifundisha, hatutakiwi kukata tamaa,” alisema Lechantre.


Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.

No comments