KIWANGO CHA FEDHA KILICHOTUMIKA KWA USAJILI WA WACHEZAJI WOTE WA SIMBA MSIMU HUU NI SAWA NA THAMANI YA MCHEZAJI HUYU WA AL MASRY.
UNAWEZA kuhisi Al Masry walikosea kumuanzisha, Ahmed Gomaa na
kumuweka nje Aristide Bance kwenye mechi yao ya juzi Jumatano dhidi ya Simba,
lakini usichokijua ni kwamba straika huyo thamani yake inazidi kiwango cha
fedha ambacho kilitumika kwa usajili wa wachezaji wote wa Simba msimu huu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt.com, bei ya Gomaa
mwenye umri wa miaka 29 sokoni kwa sasa ni Euro 600,000 (Sh1.7 bilioni) ambazo
zingeweza kusajili kikosi chote cha Simba na chenji ikabaki. Kiasi cha fedha
ambacho Simba imekitumia msimu huu kwa ajili ya kusuka kikosi chake
kinachoongoza Ligi Kuu Bara kinakadiriwa kufikia Sh1.3 bilioni.
Hii inamaanisha kwamba kama Al Masry watamuuza Gomaa leo hii,
mkwanja watakaovuta wanaweza kusajili kikosi chote cha Simba kilichocheza dhidi
yao hiyo juzi. Kama hujamfahamu bado, Gomaa ni yule aliyevalia jezi namba 15 na
ndiye aliyefunga bao la kusawazisha la Masry katika dakika ya 11.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao huo, kiwango hicho cha fedha
ambacho kinatajwa kama thamani ya Gomaa sokoni kwa sasa, kinamfanya awe
mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi cha Al Masry akifuatiwa na beki raia wa
Ivory Coast, Mohammed Koffi huku Mohammed Hamdi, Ahmed Shokry, Ahmed Ayman na
Farid Shawky wakifuatia.
Koffi anayecheza beki wa kati, thamani yake ni Euro 500,000
(Sh1.4 bilioni), Hamdi na Shokry kila mmoja akiwa na thamani ya Euro 400,000
(Sh1.1 bilioni) wakati Shawky na Ayman wakiwa na thamani ya Euro 300,000 (Sh837
milioni).
Katika hali ya
kushangaza, mshambuliaji Aristides Bance ambaye ujio wake na kikosi hicho
ulikuwa gumzo, hayupo hata katika orodha ya wachezaji watano wanaoongoza kwa
thamani kubwa kwenye kikosi cha Al Masry.
Thamani ya Bance kwenye kikosi hicho kwa sasa ni Euro 200,000
(Sh558 milioni) fedha ambazo zinaweza kulipa mishahara ya Simba kwa miezi
minne.
Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza
kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.
Post a Comment