Makala:Neymar anailambisha dunia asali kwa ncha ya kisu
Na:ABDUL MKEYENGE
NEYMAR Santos Jr ameiweka dunia ya soka kwenye viganja vyake viwili. Anaitawala kadri anavyojisikia.
Katika kipindi hiki ambacho Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanaendea ukingoni mwa soka lao, polepole Neymar ameonekana kuwa mbadala wao. Kijana anakuja kwa kasi ya ajabu.
Katika dunia hii ya leo ambayo ukimtoa Messi na Ronaldo, unadhani nani mwingine anayefuata? Ni Neymar. Kijana mmoja wa Kibrazil aliyezifanya ndoto zake zigeuke kuwa kweli.
Neymar ameiweka dunia ya soka kwenye himaya yake. Hajali watu wanasema nini juu yake, anachokifanya ni kuitikisa dunia yenyewe kadri awezavyo ili kulitunisha pochi lake. Hataki kitu kingine.
Neymar staa. Ana mvuto. Mzuri. Anamiliki ndege zake binafsi za kifahari. Ana pesa nyingi, lakini muda huu ambao wakina Messi wanakaribia kukutwa na jua la utosi ameamua kujitokeza hadharani kujionyesha kama yeye ni mfalme mpya ajaye. Hakuna wa kumpinga.
Leo angewaambia hivi PSG, kesho angewaambia vile Real Madrid, siku tatu baadae angetoa kauli tata kuhusu urejeo wake Barcelona. Huyu ndiyo Neymar version nyingine ya David Beckham katika soka.
Wakati dunia ikiamini Neymar amefika ndani ya PSG kwa kusaini mkataba mnono wa miaka mitano mwanzoni mwa msimu huu, tukiwa katika robo tatu ya mkataba wake kwa mwaka mmoja ameitikisa PSG akiwaambia wamuongezee mshahara, la sivyo ataondoka. Kauli hii ya imewafanya matajiri wa PSG kukuna vichwa vyao kila wakati kana kwamba wamepatwa na chawa kichwani. Amewashika pabaya
Katika dili hili nyuma ya pazia kuna mtu wa kuitwa Neymar Sr. Huyu ni baba yake Neymar ambaye ndiye wakala wake. Kwa pamoja Neymar Jr na Neymar Sr wameamua kuwakolofisha PSG.
Neymar Sr akihojiwa juu ya taarifa za mteja wake hakanushi wala hathibitishi na majibu yake ni mepesi tu. Juzi aliulizwa vipi mustakbari wa mtoto wake kuhusu PSG, aliwajibu waandishi tungoje lolote lile linaweza kutokea na kuongeza kuwa Neymar yuko PSG na ana furaha ya kuwepo hapo.
Haya ni majibu tata. Waarabu wa PSG wamepagawa na majibu haya. Katika zama hizi ambazo pesa za soka zimechukua hatamu duniani, unadhani Neymar alifuata soka PSG na kuikacha Barcelona?
Pesa imekuja kuharibu taswira na heshima ya soka. Miaka 15 iliyopita Ronaldinho Gaucho alitoka PSG kujiunga Barcelona, lakini miaka 15 baada ya uhamisho huo Neymar ametoka Barcelona kujiunga PSG. Fedha za soka zimetufikisha hapa.
Ile dhana ya mchezaji kujisikia fahari kuzichezea Barcelona, Real Madrid, AC Milan imeshapitwa na wakati siku hizi. Fedha imekuja kuzishushia heshima na thamani timu hizi.
Wiki moja iliyopita kiungo mshambuliaji wa Brazil Oscar Emboaba amesema hajisikii unyonge kutokuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kitakachokwenda Urusi kushiriki Kombe la Dunia baadae.
Oscar anayecheza soka lake nchini China amesema hajisikii vibaya kutokana na kupata pesa nyingi nchini humo, tofauti na Kombe la Dunia ambako mchezaji akicheza anapata heshima. Tumefikia sehemu mbaya. Leo hii mchezaji hajisikii fahari kushiriki Kombe la Dunia kutokana na pesa?
Kitendo cha Neymar siku hizi kuzitaja mara nyingi zaidi Madrid na Barcelona, kitamuingizia pesa nyingi nyingine mwishoni mwa msimu huu. Liamini hili!
Binafsi natamani nisimuelewe Neymar kwa hiki anachokifanya sasa, lakini sina budi kumuelewa.
Katika wakati huu ambao yuko majeruhi na kapumzika kwao Brazil, tujue kabisa Neymar anaionjesha asali dunia kwa ncha ya kisu.
Post a Comment