TANZANIA KUWAKILISHWA AN MUOGELEAJI MMOJA MICHUANO YA JUMUIYA YA MADOLA NCHINI AUSTRALIA

Chama cha mchezo wa kuogelea nchini (TSA) kimesema Tanzania itawakilishwa na Muogeleaji Mmoja badala ya wawili kama ilivyppangwa hapo awali katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika mapema mwezi ujao nchini Australia.




Akizungumza na Eatv Saa Moja, Mkufunzi wa mchezo wa kuogelea hapa nchini Alexander Mwaipasi amesema, walishakamilisha maandalizi kwaajili ya waogeleaji hao ambao ni Hilal Hilal na Sonia Tumiyoto lakini muogeleaji mmoja ambaye ni Sonia amepata matatizo ambayo yamemlazimu kutokushiriki mashindano hayo huku akiongeza kuwa wanaimani na muogeleaji aliyebakia kwani yupo katika maandalizi mazuri kwaajili ya kulitangaza Taifa kupitia mashindano hayo.


“Katika Michuano ya Jumuiya ya Madola tutapeleka muogeleaji Mmoja pekee ambaye ni Hilal Hilal kutokana na matatizo ya Kifamilia aliyoyapata muogeleaji wa Kike Sonia Tumioto ambayo yapo nje ya uwezo wa chama lakini Hilal amejiandaa vya kutosha na tunaamini atakwenda kufanya vizuri japo tunasikitika kumkosa Sonia ambaye naye tulikuwa tunaamini naye amejiandaa vizuri na angeweza kufanya vizuri pia kama ilivyokuwa kwenye mashindano mbalimbali, ” amesema.


Wakati huohuo Mwaipasi amesema, muitikio mdogo kwa washiriki katika mashindano ya Taifa ya mchezo wa kuogelea yaliyofanyika Machi 24 na 25 yamechangiwa na uboreshwaji wa mashindano hayo ambapo wameongeza kiwango cha kufuzu kushiriki mashindano ya taifa ili kuwa na waogeleaji bora zaidi.


“Mashindano ya Taifa kwa mwaka huu yamekuwa na idadi ndogo ukilinganisha na miaka mingine, miaka mingine tulikuwa tukipata washiriki wasiopungua 200 lakini kwa mashindano ya mwaka huu tumepata washiriki 150 na hii sio kwasababu wachezaji wamepungua hapana ila ni kwasababu tumeboresha mashindano na kuyafanya kuwa magumu kiwango cha kufuzu tumekiongeza kwahiyo imesaidia kupunguza idadi ya waogeleaji ambao bado hawajafikia viwango, ” amesema.

Mwaipasi ameongeza kuwa kwasababu ya kuweka vigezo vya kuwa na muda maalumu wa kushiriki mashindano ya Taifa imesaidia kuboresha mashindano na kuweza kupata waogeleaji wenye viwango vya juu ambao wataweza kuingia kambini mapema kwaajili ya maandalizi ya mashindano ya Dunia yatakayofanyika Desemba mwaka huu nchini China.


No comments