UONGOZI MBAO FC WASHANGAZWA NA MATOKEO YA VPL,WAKANUSHA KUTOKUWALIPA WACHEZAJI MISHAHARA.




Mara baada ya kupoteza michezo minne mfululizo ikiwemo wa jana ambao walipoteza dhidi ya Azam FC kwa bao 2-1 Klabu ya Mbao FC imesema bado inashangazwa licha ya pointi walizonazo lakini hawapo nafasi ya mwisho hivyo wanaamini hawawezi kushuka daraja. 


Mwenyekiti wa Mbao FC Solly Njashi amesema, kufungwa ni sehemu ya mchezo na pia imechangiwa na safari nyingi ambazo zimesababisha uchovu kwa wachezaji lakini wanahitaji kuongeza nguvu ili kufanya vizuri kwa michezo iliyobakia.

"Mimi kitu ambacho kinanishangaza ni kwamba tumefungwa michezo mingi sana lakini bado hatujawa wa mwisho, na naimani kabisa kama tumemaliza mechi ya jana na hatujawa wa mwisho na mizunguko tuliyokuwa nayo basi naimani tunakwenda kufanya vizuri na mashabiki wetu waendeleze umoja, " amesema. 


"Kufungwa ni sehemu ya mchezo kwasababu katika soka huwezi kwenda na matokeo yako mkononi, unaenda kupambana Uwanjani lakini mkumbuke kwamba mechi za ugenini zinakuwa ngumu na inachangiwa na safari nyingi, " amesema. 

Njashi amesema,  bado wanavijana ambao umri wao bado haujawa vizuri katika kupambana na mechi za ugenini zinawasumbua hivyo wanaamini bado wanamuda wa kuongeza nguvu ili kushinda mechi zinazofuata. 

Wakati huohuo Njashi amekanusha suala la kutolipwa mishahara kwa wachezaji ndio liachangia timu kutofanya vizuri ambapo ameongeza kuwa ni miezi miwili pekee ndio hawajawalipa wachezaji na kauli hizo zinazotolewa na baadhi ya wadau wa soka haziwezi kufelisha mikakati yao ya kuiweka timu katika sehemu imara zaidi. 


"Changamoto ya mishahara ni sehemu ya timu nyingi na sio Mbao pekeyake utakuta hata timu kubwa zipo kwenye changamoto hizi, na katika mpira wetu inaeleweka wazi kwamba tunaendesha katika utaratibu upi, na Mbao hatujawalipa wachezaji wetu kwa miezi miwili na tumejitahidi sana na tutaendelea kupambana na hilo kuhakikisha kwamba haliwezi kutokea, " amesema. 

"Labda nizungumze tu, kunakauli nyingi zinatoka lakini nadhani kunawatu wanamikakati yao juu ya Timu ya Mbao lakini nasema wazi hawatakaa waifelishe kwamipango tuliyonayo sisi, na naimani sisi hatuwezi kusikiliza nani anasema nini ila tumesimama kwenye mipango yetu tuliyonayo kuhakikisha kwamba Mbao tunaitoa hapa ilipo kwenda mahala kwingine, " amesema.

Follow us on Instagram @Tiktaktz ili uwe wa kwanza kupata taarifa mpya za michezo yote ndani ya nchi na nje ya nchi.


No comments