YANGA YATANGAZA KUIKIMBIA SIMBA KAGAME


Uongozi wa Yanga umethibitisha kuwa haitoshiriki michuano ya kombe la Kagame ambayo wamepangwa kundi moja na watani wao Simba.

Miamba hiyo ilipangwa pamoja kundi C ambapo wangekutana Julai 5 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga haipo katika kiwango bora kwa sasa na juzi walitolewa kwenye michuano ya SportPesa Super Cup kwa kufungwa mabao 3-1 na KK Homeboyz hivyo maamuzi hayo yanachukuliwa kama kuwakimbia watani wao.

Msemaji wa klabu hiyo, Dismas Ten amesema tayari wamepeleka barua Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kuthibitisha kujitoa kwao.

Ten amesema wana sababu nyingi zilizowafanya kujitoa lakini kubwa ni kuwapumzisha wachezaji ambao wamecheza mechi nyingi mfulizo.

"Ni kweli hatutashiriki michuano ya Kagame na Katibu mkuu ameandika barua na kuipeleka TFF kuwaambia tumejitoa katika mashindano.

"Kikubwa ni kuwapumzisha wachezaji ambao wamecheza mechi nyingi mfululizo, tumeona hata kama tungeshiriki tusingefanya vizuri," alisema Ten.

No comments