Makala:Ninachokianini kwa Ammy Ninje
Na:IBRAHIM SHABAN
AMMY Ninje inawezekana akawa mwalimu mzuri asiyeeleweka machoni mwa Watanzania. Ninje huyo huyo anaweza kuwa mwalimu wa hovyo ambaye Watanzania hawamuelewi na hawataki kumuelewa. Yote mawili yanawezekana.
Ninje kocha wa timu ya taifa vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) yuko kwenye kipindi kigumu kutokana na matokeo ya timu yake dhidi ya Congo DR. Matokeo yalikuwa sare tasa.
Sare hii imewatoa kusilojulikana Watanzania ambao hawachoki kumshukia kila mara. Ukipita mtaani na kuamua kukusanya maoni ya Ninje, abaki au aondoke, majibu mengi yatakuwa hafai. Ni wachache wanaomuamini Ninje.
Matokeo ya Kilimanjaro Stars kule Kenya mwishoni mwa mwaka jana ni sehemu nyingine inayotumiwa kama fimbo ya kumchapia Ninje. Namuonea sana huruma.
Kuna kitu nakiamini kupitia Ninje huyu anayeonekana mwanadamu wa tofauti nyusoni mwa Watanzania wenzake.
Ninje ni kocha mzuri sana tena sana, lakini shida yake ni kutofahamu vyema mahitaji ya mpira wa Kitanzania.
Ninje ni Mtanzania kama walivyo Watanzania wengine. Muda wake mwingi wa kujifunza ukocha amejifunza nje anaporudi nyumbani hapati jopo kubwa lililomzunguka kwa ajili ya kurahisisha kazi zake ziwe rahisi. Ninje haeleweki hapa tu!
Mfano rahisi ni hii Ngorongoro aliyonayo sasa hivi. Wakati timu hii ikikusanywa yeye (Ninje) hakuwepo nchini, amekuja na kuikuta timu ishaitwa. Nani aliwaona wachezaji hawa na kumuitia Ninje?
Hili ndiyo kosa ambalo Ninje anahukumiwa nalo. Katika benchi lake la Ngorongoro ana Leopard Tasso Mkebezi, Boniface Pawasa na John Mashaka. Hawa ni watu wanaofahamu vyema mpira wa Tanzania, lakini wanatosha kumsaidia Ninje?
Mkebezi amewahi kuwa staa mkubwa nchini, Taifa Stars ilipofuzu Mataifa Afrika 1980 Nigeria. Mara mwisho kuwa karibu na mpira wa miguu ni kuwa Meneja wa Taifa Stars ilipokuwa chini ya Marcio Maximo. Muda mrefu hakuwa nasi mpirani.
Pawasa ni mmoja ya walinzi mahiri wa Tanzania waliowahi kutokea. Katika kikosi hiki ana kazi ya kujenga phiysical za wachezaji. Ni wapi Pawasa alisomea somo hili?
John Mashaka. Hapa ndiyo kwenye kituko kabisa. Huyu jamaa muda mwingi wa michezo ya Ligi Kuu au kimataifa anakuwa mlinzi wa magetini, mtu huyu anaongeza kitu gani kwa Ninje? Ninje ana mengi yanayomferisha, ila mwisho wa siku anaonekana yeye kama kocha mkuu wa kikosi.
Kama selection hii ya timu angeifanya Ninje mwenyewe na akapewa jopo mahiri la kumsaidia angeweza kufanya kitu kama alivyofanya huko Uingeereza.
Lakini kwa hiki anachokutana nacho, sioni wimbo wa lawama ukiacha kuimbwa midomoni mwa watu. Ataimbwa sana.
Post a Comment